
Bukhari ameandika ndani ya Sahih yake katika juzuu ya nane Kitabul-tauhid mlango wa kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo, Malaika na Roho hupanda kwake kwamba, Ali ibn Abi Talib alipokuwa Yemen alimtumia Mtume (s.a.w.w) kipande cha dhahabu, Mtume akakigawa kwa baadhi ya watu, basi Maquraish na Maansar wakakasirika na wakasema: "Anawapa wakuu wa watu wa Najd na anatuacha sisi? "Mtume (s.a.w.w) akasema: "Hakika nawaimarisha nyoyo zao." Akaja mtu fulani akasema: "Ewe Muhammad muogope Mwenyezi Mungu." Mtume akasema, "Ni nani basi atakayemtii Mwenyezi Mungu iwapo mimi nitamuasi" Mwenyezi Mungu Ameniamini kunituma kwa walimwengu, ni vipi ninyi hamuniamini.?"
Khalid ibn Walid akaomba amuue mtu huyo, Mtume (s.a.w.w) akamkataza kufanya hivyo, basi mtu yule alipoondoka Mtume (s.a.w.w) akasema: "Bila shaka katika asili ya huyu kuna watu wanasoma Qur'an lakini haingii nyoyoni mwao na wanatoka katika Uislamu kama utokavyo mshale kwenye upinde na wanawauwa Waislamu na kuwaacha watu wa Masanamu, basi lau nitawadiriki nitawaua mauaji ya Adi."
Rejea: Sahih Bukhar J.8 Uk. 178
Huyu ni mnafiki miongoni mwa Masahaba, anamtuhumu Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa anafanya dhulma katika mgao na anamkabili Mtume bila ya Adabu kwa kumwambia: "Ewe Muhammad muogope Mwenyezi Mungu." Lakini pamoja na kuwa Mtume anaufahamu unafiki wa mtu huyu na kwamba watatoka katika asili yake watu watakaotoka ndani ya Uislamu kama utokavyo mshale kwenye upinde, na watauwa Waislamu na kuwaacha watu wanaoabudu Masanamu, pamoja na yote hayo Mtume anamzuiya Khalid asimuue mtu huyo
Bukhar ameandika ndani ya Sahih yake katika juzuu ya nne mlango unaohusu vitu alivyokuwa akiwapa Mtume wanaoimarisha nyoyo zao, katika Kitabul-Jihad, Was-sair, kutoka kwa Abdallah (r.a) amesema: "Ilipokuwa siku ya Hunain Mtume aliwaboresha watu fulani katika mgawo, akampa Aqrau ibn Habis ngamia mia, na akampa Uyaynah hivyo hivyo, na watu wengine miongoni mwa mabawana wa Kiarabu siku hiyo akawatangulia katika mgao, basi mtu mmoja akasema: "Namuapa Mwenyezi Mungu mgao huu hauna uadilifu ndani yake na wala haukukusudiwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu." Mimi nikasema: "Wallahi nitamwambia Mtume." Kisha nikamfuata na nikamwambia, akasema: "Ni nani mwingine atakayefanya uadilifu ikiwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakufanya uadilifu? Mwenyezi Mungu amrehemu Mussa aliudhiwa zaidi kuliko haya lakini alivumilia."
Rejea: Sahih Bukhar J.4 Uk. 61
Huyu ni mnafiki miongoni mwa Masahaba wa Mtume (s.a.w.w) na huenda alikuwa miongoni mwa mabwana watukufu wa Kiquraishi, na utamuona mnafiki huyu anaamini kabisa kwamba Muhammad hakuwa muadilifu na wala hakukusudia radhi za Mwenyezi Mungu katika mgao wake. Mwenyezi Mungu amrehemu Muhammad aliudhiwa zaidi ya haya na akavulimilia.