VIZITO VIWILI.

Bismillah Rahmanr Rahiim.

Kwa miaka kadhaa sasa na hasa baada ya Mapinduzi ya Kiislam ya 1979 huko Iran. kumekuwa na juhudi kubwa za kushawishi Ummah wa Kiislam kuwa Shia sio Waislam, bali ni makafiri. Juhudi hizo zimekuwa zikiongozwa na zinaongozwa hadi sasa na Masheikh wa Kiwahhabi (Answaru Sunna). Mihadhara mingi imefanywa na vitabu vyingi vimeandikwa. Baadhi ya watu inavyoonekana wameathiriwa na Propanganda hizo kwa kufikirishwa kwamba yanayoaminiwa na Shia hayana maana wala msingi wowote wa Kidini, isipokuwa ni mambo waliyoyatoa katika vichwa vyao! Pia Shia wametuhumiwa kuamini mambo ambayo hawayaamini bali wanayapinga kamwe! Ili kuzisahihisha fikra hizo wanazojazwa nazo watu kwa uchokozi tumekusudia katika mfululizo huu kuwaeleza Waislam yale tunayoamini kinyume na yanayoaminiwa na wengine na sababu zetu kama ilivyo katika Qur'an Tukufu na Sunnah za Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w). Baada ya hapo (Sura 49:6) uamuzi tunakuachia wewe (Sura 76:29). Ukumbuke kwamba kesho siku ya Hukumu utasimama peke yako (Sura 19:95) na imani yako na amali yako (Sura 99:7-8). Jambo la kwanza ambalo Shia Huhitalifiana na wasio Shia ni kuhusu Uongozi baada ya Bwana Mtume (s.a.w.w), Shia wanaamini kwamba jambo hilo lilikwisha amuliwa na Mwenyezi Mungu na Tukufu Mtume (s.a.w.w) kabla ya kuaga dunia kwamba:
1- Khalifa wa Waislam wanatokana na Ahlul-Bayt a.s (Watu wa Nyumba ya Mtume s.a.w.w)
2- Wote kwa ujumla watakuwa kumi na wawili
3- Wa kwanza wao atakuwa Ali bin Abi Talib (a.s).
Sasa tuangalie mategemeo yao.
Kuthibitisha kwamba makhalifa Maimamu watatokana na Ahlul-Bayt (a.s). Shia utegemea Hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w) zinazoeleza hivyo, na ambazo hupatikana hata katika vitabu vya wale wanaolikataa hilo kwa mfano:
1- Katika Sahih Muslim imeandikwa kwamba Zayd bn Arqam Amesema kuwa Mtume (s.a.w.w) alisema: "Enyi watu! Hakika mimi ni binadamu nami nataraji (hivi karibu) kujiwa na mjumbe (Malaika wa Mauti wa Mola wangu na kuitika (mwito wake) kwa  hivyo nina waachia nyinyi vizito viwili cha kwanza Kitabu cha Mwenyezi Mungu chenye Uongozi na Mwangaza. Basi shikamaneni na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na watu wa Nyumba yangu (AHLUL-BAYT A.S).
Ninawakumbusha nyinyi watu wa Nyumba yangu
Ninawakumbusha nyinyi watu wa Nyumba yangu
Ninawakumbusha nyinyi watu wa Nyumba yangu
2- Katika Sunan Al-Tirmidhi imeandikwa kwamba Jibir bn Abdillahi Amesema: "Nilimwona Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w.w., Katika Hijjah yake siku ya Arafah, naye yu juu ya Ngamia wake anahutubu. Nikamsikia Anasema: "Enyi watu! Mimi ninawaachia nyinyi  ambavyo mkishikamana navyo. Hamtapotea Kitabu cha Mwenyezi Mungu na jamaa zangu watu wa Nymba yangu (AHLUL-BAYT A.S)
3- Katika Musnad Ahmed imeandikwa kwamba Zayd bn Thabit Amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu  (s.a.w.w) alisema: "Mimi nina waachia nyinyi Makhalifa wawili-Kitabu cha Mwenyezi Mungu na watu wa Nyumba yangu na kwamba viwili hivyo havitafarikiana mpaka vinirudie kwenye hodhi vyote.
Japo kuwa hapo juu tumetaja Vitabu vutatu tu, lakini kwa kweli Hadithi Hiyo-inayojulikana kwa jina la Hadith Al-Thaqalayn (Hadithi ya Vizito viwili). Imetajwa katika vitabu vingi sana vya Kisunni vya Hadith na vya Tafsiri ya Qur'an. Pia imepokewa kwa njia nyingi kama alivyosema Ibn Hajar na kwa Sahaba wasiopungua 35.
Hadith hizo zimetuwekea wazi maagizo ya Bwana Mtume (s.a.w.w) kwamba tushikamane na Ahlul-Bayt (a.s) baada yake yeye na kwamba kushikamana na wao pamoja na Qur'an Tukufu ndiko kutakakotupatia sisi uwokovu na kutopotea.

Swali: AHLUL-BAYT (A.S) NI NANI?
Vidokezo
1- Kitabu Al Fadhail Mlango wa Fadhail Ali
kwa Kiingereza ni Vol. 4 Uk 1286. Hadithi 5920
2- Juzuu ya Pili. Uk. 308
3- Juzuu ya Tano. Uk. 189
4- Katika kipambanuzi cha kwanza. Malango wa 11 wa kitabu chake kiitwacho Al-Sawaiq Al-Muhriqah. uK. 89.