SIRI NA MAARIFA YA HIJJAH KWA MTAZAMO WA IMAM ALI BIN ABI TALIB (A.S).


Hija ni safari ya siku chache lakini yenye matunda na manufaa makubwa mno. Ni safari ya siku kadhaa lakini yenye kuwa na mafunzo ya karne kadhaa. Ardhi ya Makka ambayo ni ardhi ya Wahyi, katika wakati huu hufurika makundi kwa makundi ya Mahujaji waliowafikishwa kwenda kutekeleza moja ya ibada muhimu katika dini tukufu ya Kiislamu, ibada ambayo ni wajibu kuitekeleza mara moja tu katika kipindi cha umri wa mwanaadamu. Kila mwaka katika masiku haya ya maelfu kwa maelfu ya Mahujaji kutoka kaumu, nchi, makabila na rangi mbalimbali husafiri katika ardhi hiyo tukufu na yenye nuru ili wakanufaike na chemchemi ya maarifa na imani. Kwa hakika ibada ya Hija ni harakati ya mja kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni safari ya mtu kutupilia mbali mambo yote anayofungamana nayo na kuanza maisha mapya. Kila hujaji aliyepata tawfiki ya kwenda kutekeleza ibada ya Hija anapaswa kutumia fursa hii adhimu kujitakasa kiroho na kinafsi na wakati huo huo kupata nafasi isiyo na mithili ya kuweza kupitia historia kwa macho kutokana na kutembelea maeneo yenye athari za Uislamu katika ardhi tukufu za Makka na Madina. Kwa hakika kweda kuhiji Makka ni hatua ya kuelekea katika marhala ya twaa, uja na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
Siri na falsafa ya Hija ni miongoni mwa elimu na maarifa ambayo Imam Ali AS ameyaashiria kwa maana nzuri na pana mno katika kitabu cha Nahaj al-Balagha yaani Njia ya Balagha. Miongoni mwa athari muhimu ya Hija ni kubadilika kiroho na kisaikolojia watu waliopata tawfiki ya kwenda kuhiji. Mahujaji ambao wanaidiriki Hija kwa ujudi wao wote huhisi athari ya kimaanawi na kiroho katika nyoyo zao mpaka mwishoni mwa umri wao. Pengine ni kutokana na sababu hiyo ndio maana ibada ya Hija ikawajibishwa kwa Waislamu mara moja tu katika kipindi cha umri wa mwanaadamu.
Kwa kuzingatia taathira hii, Mahuja huelekea katika nyumba ya Mwenyezi Mungu wakiwa na furaha na hali maalumu. Kila hatua moja anayopiga Hujaji huwa ni hatua ya kumkurubia Mwenyezi Mungu na maabudi wake kipenzi. Ni kutokana na sababu hiyo Hija ikahesabiwa kuwa ni kuzaliwa upya. Imam Ali bin Abi Talib AS, Imamu wa Mashariki na Magharibi anatoa taswira ya msongamano wa Mahujai wenye hamu na shauku kubwa katika Hija kwa kusema: Mwenyezi Mungu Mkubwa amekuwajibishieni Hija ambayo ni nyumba yake, nyumba ile ile ambayo ni kibla cha watu. Mahujaji huwa sawa na wenye kiu ambao wameyafikia maji, huharakisha kuingia hapo makundi kwa makundi. Allah ameifanya nyumba Yake kuwa sehemu ya kuonyesha khushui mkabala na adhama na kusalimu amri kwao mbele ya izza Yake.
Imam Ali AS anakumbusha kwamba, katika Uislamu hakuna kigezo chochote kama cha rangi, kabila, utaifa na kadhalika ambacho kinakubaliwa; bali mpaka wa mgawanyo wa watu ni itikadi juu ya Mwenyezi Mungu na haki za utukufu wa mwanadamu huku daraja ya mtu akipatiwa kulingana na uchaji wake Mungu. Kwa hakika hili linadhihirika zaidi katika Hija kuliko ibada nyingine. Katika ibada ya Hija mipaka ya kijiografia haizingatiwi, hakuna kutazama huyu ni mweupe au mweusi, mwekundu au wanjano, mzungu au mwarabu, mhindi au Muirani mwafrika au mchina. Katika ibada ya Hija hakuna tofauti baina ya masikini na tajiri, msomi au mjinga, mwenye nguvu au dhaifu kwani wote huwa katika vazi moja tu nalo ni vazi tukufu la Ihramu, tena vazi jeupe la kawaida mno na ambalo halina ufakhari. Mahujaji huwa wageni wa Mwenyezi Mungu katika nyumba Yake Tukufu wakiwa na vazi hilo la Ihramu na huwezi kutofautisha yupi ni tajiri au masikini kati yao. Kwa hakika huu umoja wa itikadi ni msimu bora kabisa wa pamoja wa Waislamu ulimwenguni. Wakiwa Makka, mahujaji hufanya jitihada za kukata mafungamano yao yote ya kimaada, kama vyeo, kazi, mali, hadhi na daraja zao za kidunia na kidhahiri.
Mahujaji wakiwa Hija hufanya jitihada za kutaka kutambua hakika ya dhati zao mbali kabisa na mapambo ya kidhahiri ya kidunia. Kwa maana kwamba, mwanadamu ambaye amekumbwa na mghafala juu ya hakika ya dhati yake kutokana na kugubikwa na mambo ya kimaada, huweza kuona hakika ya nafsi yake katika kioo cha vazi la Ihramu na kuvua nguo za kidhahiri za kidunia na pia kutambua nakisi na mapungufu yake. Hujaji anayevua nguo zake za kawaida na kuvaa vitambaa viwili vyeupe vya Ihramu hufahamu kwamba anapaswa kuvua na kutupilia mbali guo na vazi la kiburi, ghururi, maasi na mapambo ya kidhahiri ya kidunia. Imam Ali AS anaishabihisha hali ya kufanya tawafu ya Mahujaji walio na nyoyo zilizofungamana na tawafu ya wakazi wa arshi ya Mwenyezi Mungu na kusema: Wao wameshabihiana na Malaika ambao wanazungumza na kufanya tawafu katika arshi ya Mwenyezi. Kwa mtazamo wa Imam Ali AS, Waislamu ambao wamefanikiwa kutekeleza ibada ya Hija, kwa hakika wamepiga hatua katika njia ya Mitume AS na kuungana katika daraja ya uja ya waja hao wa Mwenyezi Mungu. Mbali na ibada ya Hija kuwa na nafasi muhimu katika suala la kuonyesha adhama ya Waislamu, umoja na masuala mengi ya kimaanawi, imekuja katika Uislamu kwamba, Hija inaweza kuongeza nguvu ya kiuchumi ya Waislamu. Hapana shaka kuwa, tatizo kubwa la Waislamu hii leo ni kufungamana kwao na kuwa tegemezi uchumi wao kwa wageni. Endapo pambizoni mwa Hija kutaandaliwa makongamano na warsha kubwa za wasomi wa uchumi katika ulimwengu wa Kiislamu na wataalamu wa iktisadi ili kujadiliana na kutafuta njia ya kuwakomboa Waislamu kutoka katika makucha ya umasikini na kuwa tegemezi kwa wageni sanjari na kupendekezwa njia mwafaka, hapana shaka kuwa, Ulimwengu wa Kiislamu unaweza kustafidi na vyanzo vingi vya utajiri ulivyonavyo na kuuondoa Umma wa Kiislamu katika umasikini.