TAHADHARI KUHUSIANA NA HATARI YA HARAKATI ZA UZUSHAJI FITNA NCHINI IRAQ.


Kufuatia kushadidi mashambulio ya kigaidi nchini Iraq, na katika hatua yenye lengo la kuinasua nchi hiyo na mgogoro unaoendelea hivi sasa, shakhsia kadhaa wa kidini na kisiasa wa Iraq wameitahadharisha mirengo mbalimbali ya Kiiraqi na kauli za kuchochea mifarakano. Ammar al Hakim, Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq ametahadharisha kuhusu matamshi na hatua za kuchochea mifarakano, na kuwataka maulamaa wa Iraq na wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla wawaelimishe wananchi juu ya hatari ya mienendo hiyo. Kwa mujibu wa Ammar al Hakim hatari ya kuchochea mifarakano baina ya Waislamu haiikabili Iraq peke yake, bali njama hiyo inatishia maslahi ya umma mzima wa Kiislamu. Ayatullah Ali Sistani, kiongozi mkuu wa kidini wa Waislamu wa Kishia nchini Iraq amesisitiza kwamba yanayojiri hivi sasa ndani ya umma wa Kiarabu na wa Kiislamu kwa ujumla, na hasahasa nchini Iraq hayakubaliki mbele ya Waislamu, na kwamba kila mtu anapaswa kufanya jitihada za kutatua hitilafu zilizopo. Ayatullah Sistani amewataka Wairaqi wote wadumishe umoja na mshikamano na kuweka kando mielekeo ya kikoo. Naye Waziri Mkuu Nouri al Maliki ametahadharisha juu ya kurejea fitna za kikoo na kimatapo nchini humo na kueleza kwamba ikiwa fitna za kikoo na kimatapo zitaendelea, Iraq itakabiliwa na hatari ya kugawanyika.

Tangu mwanzoni mwa mwaka uliopita wa 2012 hadi sasa mikoa ya al Anbar ulioko magharibi, Nainawa, Salahuddin na Kirkuk iliyoko kaskazini na mkoa wa Diyala ulioko mashariki mwa Iraq imegeuka kuwa uwanja wa machafuko na maandamano ya kupinga serikali, huku baadhi ya hotuba za Sala ya Ijumaa zinazotolewa katika maeneo hayo zikihamasisha hisia za kikoo na kuwafanya baadhi ya watu waitumie anga ya hisia hizo iliyotanda nchini humo kwa manufaa yao. Katika hali kama hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, amesema ametia wasiwasi na machafuko yaliyojiri katika siku kadhaa zilizopita nchini Iraq na kupelekea kuuliwa makumi ya watu na hivyo kuvitaka vikosi vya usalama vya nchi hiyo vifanye jitihada ukomo wa uwezo wao ili kurejesha nidhamu na kusimamia sheria nchini humo. Aidha amesisitiza kwamba vyovyote itakavyokuwa maandamano ya wapinzani yanapasa yafanyike katika mazingira ya amani. Wakati huohuo Wizara za Mambo ya Nje za Iran na Russia zimetoa taarifa ya kulaani mashambulio ya kigaidi nchini Iraq na kusisitiza kuwa kuitumia vibaya makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka hali inayotawala nchini Iraq ili kuvuruga zaidi uthabiti wa nchi na kuchochea hitilafu za kimadhehebu kati ya Mashia na Masuni, kunatia wasiwasi mkubwa.
Mbali na kukabiliwa na mgogoro wa kisiasa na mivutano kati yake na baadhi ya makundi ya kisiasa, serikali ya Baghdad, kwa miezi kadhaa sasa inakabiliana pia na maandamano yanayofanyika katika baadhi ya maeneo ikiwemo mikoa ya al Anbar, Nainawa na Salahuddin ya kulalamikia watu wanaoendelea kuwekwa kizuizini pamoja na madai mengine waliyonayo wananchi kwa serikali yao. Hata hivyo badala ya kuchukua sura ya kubainisha matakwa ya wananchi, maandamano hayo, zaidi yamekuwa na mielekeo na utashi wa kikoo na kikaumu. Kwa mara kadhaa, serikali ya Iraq imetoa wito kwa makundi ya kisiasa kukaa kwenye meza ya mazungumzo na kufanya jitihada za kutatua hitilafu zilizopo kwa njia za kisiasa na maelewano. Aidha sambamba na kuashiria uingiliaji wa baadhi ya nchi za Kiarabu pamoja na Uturuki katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, serikali ya Waziri Mkuu al Maliki imekuwa ikisisitiza kwamba njia yoyote ile ya kuinasua nchi na mgogoro uliopo inahitajia kwanza kurejea utulivu nchini, na kwamba hilo halitawezekana bila ya kufadhilisha na kutanguliza mbele maslahi ya kitaifa ya Iraq badala ya utashi na maslahi ya kikoo…/ Kutoka  http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/31579-tahadhari-kuhusiana-na-hatari-ya-harakati-za-uzushaji-fitna-nchini-iraq