MASHIA NA MASUNNI IRAQ WASWALI IJUMAA PAMOJA.
Maelfu ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni nchini Iraq leo
wamesimamisha sala ya Ijumaa pamoja kama njia ya kuimarisha umoja wa
Kiislamu na kupinga mapigano ya kimadhehebu nchini humo.
Waislamu wa Iraq wameungana katika Sala ya Ijumaa katika maeneo mbali
mbali nchini humo kufuatia wito wa Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al Maliki
ambaye amewataka Wairaqi Mashia na Masunni kuswali pamoja kama njia ya
kusisitiza udharura wa umoja na mshikamano nchini humo.
Televisheni za Iraq zimeonyesha wanazuoni, wanasiasa na wananchi kutoka
madhehebu ya Shia na Sunni wakiwa wamesimama pamoja katika safu za sala
ya Ijumaa ili kuvunja njama za maadui ambao wamekuwa wakiibua hitilafu
baina ya Waislamu nchini humo. Katika siku za hivi karibuni Iraq
imeshuhudia hujuma za kigaidi ambapo mamia ya watu wamepoteza maisha.
Magaidi hao wamekuwa wakiwalenga maafisa wa usalama na misikiti.