IRAN YAIKOSOA JAMII YA KIMATAIFA KWA KUNYAMAZIA UNYAMA DHIDI YA WAISLAMU WA MYANMAR.



Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza Kuu la umoja huo kuitisha kikao maalumu kwa shabaha ya kujadili hali ya Waislamu wa Myanmar. Muhammad Khazaei amesema hayo katika kikao cha mabalozi na wawakilishi wa kudumu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na kusisitiza kwamba, hatua zozote zile za kufuta jamii fulani au wafuasi wa Uislamu nchini Myanmar si za kimantiki na haikubaliki kwa kisingizio chochote kile kiwacho. Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema, hatua hizo hazisameheki na kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kila upande kwa ajili ya kusitisha unyama na jinai zinazofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Ameongeza kuwa, nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC zinapaswa kujitokeza na kuitaka serikali ya Myanmar isitishe ukiukaji wa haki za binadamu na vitendo vya kinyama dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Khazaei pia sambamba na kukaribisha kwa mikono miwili hatua ya kuundwa Kundi la Mawasiliano la OIC kwa ajili ya kufuatilia hali ya Waislamu wa Myanmar amesema bayana kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataraji kuona kukichukuliwa hatua, kufanyika uchunguzi na kufanyiwa kazi ripoti ya kundi hilo la mawasiliano. Amesema, Iran ikiwa Mwenyekiti wa Kiduru wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM inafutailia pia suala hilo katika asasi za kimataifa. Kuna karibu Waislamu laki nane wa jamii ya Rohingya magharibi mwa Myanmar ambao wamenyimwa kabisa haki zao za kiraia, na ni miezi kadhaa sasa ambapo wamekuwa wakikabiliwa na mashambulio ya Mabudha makatili na wenye misimamo ya kupindukia. Serikali ya Myanmar nayo imeng'ang'ania msimamo wake ule ule kwamba, raia hao wa jamii ya Rohingya ni wahajiri wa Kibangladeshi na kwamba, sio raia wa Myanmar. Hadi sasa mamia ya Waislamu wa Rohingya wameuawa ikiwa ni natija ya vitendo vya kinyama dhidi yao vinavyofanywa na Mabudha nchini humo, huku maelfu ya wengine wakilazimika kuwa wakimbizi. Katika hali ambayo ubainishaji wa uhakika wa mambo na hali halisi ya takwimu na unyama wanaofanyiwa Waislamu wa Myanmar limekuwa likizuiwa; siku chache zilizopita kuliripotiwa habari ya kuzama boti iliyokuwa imewabeba wakimbizi 200 wa Rohingya wanaokimbia nchi hiyo ili kusalimisha roho zao. Mtu mmoja tu alisamika huku waliobakia wote wakizama na kupoteza maisha yao baada ya boti yao kupigwa na tufani baharini. Licha ya jinai hizo kuendelea kufanywa mchana kweupe dhidi ya Waislamu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekataa hata kutuma tu kamati ya kuchunguza ukweli wa mambo nchini Myanmar, hatua ambayo kama ingefanyika bila shaka ingefichua zaidi dhulma, unyama na ukatili wanaofanyiwa Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo. Ni kwa kuzingatia hali hiyo mbaya inayowakabili Waislamu wa Myanmar, ndio maana Muhammad Khazaei, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa akataka Ban Ki-Moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa au mwakilishi wake aalikwe katika kikao maalumu cha Baraza Kuu la umoja huo ili aje kutoa ripoti kuhusiana na hali ya Waislamu nchini Myanmar. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/31973-iran,-waialamu-mynamar,-jamii-ya-kimataifa,-kunymazia,-rohingya,mauaji,-mabudha