IMAM ALI BIN ABI TWALIB (A.S), SAUTI YA UADILIFU.

Bismillahir Rahmanir Rahim

Wanahistoria wa Kiislamu wanasisitiza kuwa moja ya sifa za Imam Ali bin Abi Twalib (AS) ilikuwa ni kutekeleza sheria za Mwenyezi Mungu bila ya kujali yasemwayo au lawama za wanaolaumu.

Ibnu Abil Hadid al Muutazili amenukuu katika Sherhe ya Nahjul Balagha kwamba baada ya kushika hatamu za uongozi, Amirul Muuminin (AS) alichukua hatua za dharura za kujaribu kuboresha hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya Waislamu na kutekeleza uadilifu na usawa kama hali ilivyokuwa katika zama za Nabii Muhammad (SAW). Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Sayyidul Ausiya ilikuwa ni kufuta mfumo uliokuwa ukitumiwa na makhalifa walioongoza kabla yake wa ugawaji wa mali na pato la taifa. Alianza kutekeleza usawa na uadilifu wa kipindi cha Mtume wa Rehma Muhammad (SAW). Alisimama mbele ya watu na kusema kama inavyonukuliwa katika kitabu cha Nahjul Balagha kwamba: "Enyi watu! Kila mtu katika Muhajirina na Ansari katika masahaba wa Mtume (SAW) anayejiona kuwa bora kuliko watu wengine basi anapaswa kuelewa kwamba ubora halisi utaonekana kesho mbele ya Mwenyezi Mungu na Yeye Mola Mkwasi ndiye atakayelipa ujira na thawabu zake.

Ninyi nyote ni waja wa Mwenyezi Mungu na mali hii ni mali ya Mwenyezi Mungu inayopaswa kugawanywa baina yenu kwa usawa na uadilifu. Hakuna bora zaidi kati yenu kuliko mwingine wala Mwenyezi Mungu hakuijalia dunia kuwa ujira na malipo ya wamchao." Kisha Imam Ali bin Abi Twalib alinadi mbele ya Waislamu wote na kusema kwamba kesho tutagawa mali ya Baitulmal na watu wote Waarabu na wasio Waarabu wanapaswa kuhudhuria kwenye mgao huo. Siku iliyofuata Imam alimwita karani wake Abdullah bin Abi Rafi' na kumwambia: "Anza kuwapa Muhajirina waliohama kutoka Makka. Aliwaita na kumpa kila mtu dinari tatu kisha akawaita Ansar waliowapokea Muhajirina mjini Madina na kuwapa haki yao ya dinari tatu kama Muhajirina. Imam aliendelea kugawa mali ya Waislamu kwa watu wengine wote dinari tatu tatu bila ya kujali Mwarabu au Mwafrika, watu wa ngazi za juu katika jamii au masikini wa daraja la chini. Alipokaribia mtu mmoja kuchukua haki yake, Sahl bin Hunaif alisimama na kumwambia Imam Ali (AS): "Huyu alikuwa mtumwa wangu jana nimemuachia huru leo." Imam aliamuru apewe dinari tatu kama watu wengine. Baadhi ya masahaba kama Twalha, Zubair, Abudullah bin Umar, Said bin al As, Marwan al Hakama na watu wengine wa kabila la Kuraish walikataa kuhudhuria katika mgao huo wakipinga suala la kupewa hisa sawa na watu wa kawaida. Hata hivyo Imam aliendeleza mwenendo huo wa kukomesha mgao wa Baitul Mal kwa kuzingatia nafasi za kijamii za watu, ukabila na tofauti za rangi na kaumu na si kwa kutilia maanani uadilifu na usawa kama alivyokuwa akifanya Mtume Muhammad (SAW).

Imepokelewa pia kwamba wanawake wawili walimwendea Imam Ali bin Abi Twalib (AS) wakati alipokuwa akigawa mali za Baitulmal na hazina ya Waislamu. Mmoja wa wanawake hao alikuwa Mwarabu na mwingine alikuwa miongoni mwa Waislamu wasiokuwa Waarabu waliojulikana kwa jila la Mawaly. Imam aliwapa wote hisa sawa ya dirhamu 25 bila ya kutofautisha baina ya Mwarabu na mwenzake asiyekuwa Mwarabu. Mwanamke wa Kiarabu ambaye hakuzoea hali hiyo kutokana na mfumo uliokuwa ukitawala kabla ya serikali ya Imam Ali (AS) baada ya kuaga dunia Mtume Muhammad (SAW) alisema: "Ewe Amirul Muuminina! Mimi ni mwanamke Mwarabu na huyu ni Muajemi." Imam Ali (SA) alijibu kwa kusema: "Sikuona tofauti yoyote baina ya wana wa Ismail na wale wa Is'haq katika mgao wa mali hii.

Wanahistoria wamenukuu mengi mno kuhusu uadilifu usiokuwa na kifani wa Amirul Muuminina Ali bin Abi Twalib na jinsi alivyokuwa akiishi maisha ya chini na zuhudi licha ya kuwa kiongozi wa dola kubwa zaidi la dunia ya wakati huo. Alikuwa akiishi katika nyumba inayoshabihiana na za watu maskini zaidi katika jamii na chakula chake cha hali ya juu zaidi kilikuwa mkate wa shayiri iliyokuwa ikisagwa na mke wake mwema Bibi Fatima al Zahra au yeye mwenyewe. Alitosheka katika mambo ya dunia kwa nguo mbili tu zilizochoka na vipande viwili vya mkate kama anavyosema mwenyewe kwenye barua aliyomuandikia gavana wake Uthman bin Hunaif. Alijikurubisha kwa Mola Muumba kila alipoweza kufanya hivyo. Abdullah bin al Hussein bin Hassan (AS) anasimulia kwamba: "Ali bin Abi Twalib (AS) aliwaachia huru watumwa elfu moja katika kipindi cha uhai wa Bwana Mtume (SAW) kwa pesa aliyochuma kwa mikono yake na kuitolea jasho. Baada ya kuchukuwa hatamu za uongozi, hakuwa na chakula kitamu zaidi ya tende na vazi zuri zaidi kwake lilikuwa nguo ya pamba duni." Mwisho wa kunukuu.

Imam (AS) alichunga mipaka na sheria za Mwenyezi Mungu (sw) katika kila hali na hakuathiriwa na jambo lolote katika suala hilo. Imepokewa kwamba baada ya kukamilisha vita vya Jamal, Ali (AS) alienda mjini Kufa na kuingia katika Baitulmal huku akisema: "Ewe mali mguri na umhadai mwingine ghairi yangu mimi." Alianza kugawa mali hiyo kwa watu wote. Hapa alikuja mjukuu wake wa kike kutoka kwa mmoja wa watoto wake wa kiume akachukua kitu fulani katika Baitulmal na hazina ya Waislamu. Imam Ali (AS) alishika mkono wa mtoto huyo na kumnyang'anya. Baadhi ya masahaba zake walimwambia: "Ewe Amirul Muuminin, Mtoto huyo pia ana haki katika Baitulmal. Imam aliwajibu kwa kusema: "Baba yake akishachukuwa haki yake, ampe kila atakacho." Vilevile imepokelewa kwamba mtoto wa ndugu yake Ja'far bin Abi Twalib, yaani Abdullah alimwendea na kumwambia: "Yaa Amirul Muuminin, Amuru nipewe msaada na matumizi kutoka katika Baitulmal. Hakika sina chochote kwa ajili ya matumizi isipokuwa niuze mnyama wangu huyu. Imam alimjibu kwa kusema: "Wallah sifanyi hivyo katu, huna haki yoyote isipokuwa kama unataka kumuamuru ami yako aibe na kukupa wewe."
Wanahistoria wote mashuhuri pia wamesimulia kisa cha Imam Ali na ndugu yake Aqiil ambaye alikuwa kipofu.

Wanasema Aqiil alimuomba kaka yake amzidishie kibaba cha ngano kutoka kwenye hazina ya Waislamu na akakariri ombi hilo kwa Imam. Ali (AS) alichukua chuma na kukiweka kwenye moto hadi kiliposhika moto na kuwa chekundu kabisa. Kisha alikikurubisha kwenye mkono wa ndugu yake. Aqiil alipiga yowe na kushtuka na hapa Imam alimpa mawaidha akisema: "Ewe Aqiil! Unapiga mayowe kutokana na chuma kilichotiwa moto na mwanadamu kwa ajili ya mchezo tu huku ukinuburuta mimi kwenda kwenye moto uliowashwa na Mwenyezi Mungu Jabbari kutokana na ghadhabu yake! Unapiga mayowe kutokana na maumivu na unanitaka mimi nisipige mayowe kutokana na moto wa Jahannam?"

Suwaid bin Ghafla anasimulia kwamba siku moja niliingia nyumbani kwa Imam Ali bin Abi Twalib (AS) na sikukuta chochote isipokuwa mkeka uliochakaa akiwa ameketi juu yake. Nilimwambia: "Uwe Kiongozi wa Waumini! Wewe ni mtawala wa Waislamu na kiongozi wao na unamiliki Baitulmal na hazina ya Waislamu. Vilevile unatembelewa na ujumbe mbalimbali ilhali hakuna chochote nyumbani kwako isipokuwa mkeka huu?

Imam Ali bin Abi Twalib (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) alisema: "Ewe Suwaid! Hakika mwenye akili timamu haweki samani ndani ya nyumba ya kuhama (yaani dunia) huku mbele yake kukiwa na nyumba ya kuishi milele (yaani akhera). Tumehamishia huko samani na milki zetu nasi tutaelekea huko hivi karibuni." Mwisho wa kunukuu.

Sala na salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako ewe Amirul Muuminina siku uliyozaliwa, siku uliyoanguka chini msikitini ukiswali baada ya kupigwa panga kichwani na siku ukapapofufuliwa hai mbele ya Mola wako Muumba. Makala kutoka http://kiswahili.irib.ir/vipindi/item/18326-imam-ali-bin-abi-twalib-as-sauti-ya-uadilif