Harakati ya Mapambano ya Kiislamu
ya Palestina Hamas imesisitiza kuwa,
serikali iliyochaguliwa na wananchi wa Palestina ina haki ya kuingiza silaha
katika eneo la Ukanda wa Gaza.
Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema kuwa, si jinai kuingiza silaha Ukanda
wa Gaza kwani silaha hizo zinatumiwa kwa shabaha ya kujihami na mashambulizi
yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sami Abu Zuhri amesema kuwa, hakuna nchi yoyote ulimwenguni inayoweza kuzuia
kuingizwa silaha katika eneo hilo. Msemaji wa Hamas huyo amesema pia,
inasikitisha kuona kuwa, licha ya wananchi wa Palestina kushambuliwa na silaha
nzitonzito na za kisasa za utawala wa Kizayuni wa Israel, jumuiya na
taasisi za Kiarabu zimekuwa kimya na kukodoa macho Wapalestina
wakiendelea kuwekewa vikwazo, kuzingirwa na kushambuliwa kwa makombora ya Wazayuni.