WASLAMU WALIPATA USHINDI MKUBWA KATIKA VITA VYA BADR.

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema: Hakika ilikuwa ni mazingatio kwenu katika makundi mawili yaliyokutana, kundi moja lilipigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, na jingine Kafiri, likiwaona zaidi kuliko wao mara mbili kwa kuona kwa macho. Na Mwenyezi Mungu humpa nguvu amtakaye kwa nusra yake, hakika katika hayo mna mazingatio kwa wenye busara. Qur'an: 3:13

Ilikuwa tarehe 17 ya mwezi mwezi Mtukutu wa Ramadhani mwaka wa pili Hijiria, kulitokea vita kati ya Waislamu na Makuraishi. Waislamu 313 walipopigana na jeshi la Kikuraishi wapatao 950 katika (jangwa la) Badr.

Waislamu 313 kati yao 77 ni Muhajir na 236 ni Ansaar, hata hivyo Waislamu walipata ushindi mkubwa ambapo walitanguliza Mashahidi 22 kati yao 14 ni Muhajir na 8 ni Ansaar. Na wakawaua maadui 70 na kuwachukua mateka 70.

Mwenyezi Mungu anasema: "Makundi mangapi madogo wameyashinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu! Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri." Qur'an: 2:249.

Hii ni muhimu sana, inapasa kila mmoja wetu atambue kwa umakini zaidi kuwa: Ziko nguvu nyingine kubwa zaidi kuliko walizo nazo binadamu, ambazo Mwenyezi Mungu akitaka huwapa wachache wakawashinda walio wengi.

Katika tukio la Badr, Mwenyezi Mungu amelieleza kama ifuatavyo: "(Kumbukeni) mlipokuwa mkiomba msaada kwa Mola wenu, naye akakujibuni: Kwa hakika mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu moja watakao fuatana mfululizo." Qur'an: 8:9.

"Na bila shaka Mwenyezi Mungu alikusaidieni katika (Vita vya) Badr hali nyinyi ni madhalili. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru. Ulipowaambia wenye kuamini: "Je, haiwatoshi Mola wenu kuwasaidieni kwa Malaika elfu tatu wenye kuteremshwa? Kwa nini, (inawatosha) kama mkisubiri na kumcha Mungu, na watakufikieni katika wakati wao huu, atawasaidia Mola wenu kwa Malaika elfu tano wenye kushambulia kwa nguvu." Qur'an: 3:123 - 125.

Zingatia kwa umakini zaidi juu ya Aya hizi kunatajwa msaada wa Malaika elfu moja, elfu tatu, na elfu tano. Msaada ulikuwaje hasa? Ni kwamba: Kwanza Mwenyezi Mungu alileta Malaika elfu moja, kisha akaongeza Malaika elfu mbili wakawa elfu tatu, hatimae akaongeza Malaika elfu mbili wakawa jumla elfu tano.

Taz: At - Tafsirul Kaashif    J.2 Uk. 152.

Iliposemwa: "Kama mkisubiri na kumcha Mungu" Hii ni muhimu sana, inapasa kila Muumin ajue kwa makini kuwa: "Subra na Taq - wa" ndio Silaha kubwa pekee zitakazofanikisha lolote kwa hali yeyote hile.

Mtukufu Mtume (s.a.w.) alipowashauri Sahaba zake: Apigane au asipigane. Akasimama Abubakr Ibn Abi Quhafa akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika wao ni Makuraishi walio na kibri, tangu wazaliwe (mpaka sasa) hawajaamini tangu wamepata utukufu hawadhalilika, na wala hawakutoka na nia ya kupigana.
Mtume (s.a.w) akamwambia: "Keti." Abubakr. Akaketi. Mtume (s.a.w) akamuuliza Umar Bin Khattab, anaye nasemaje? Umar akasema kama yale ya Abubakr. Mtume (s.a.w) akamwambia: Keti. Umar Bin Khattab akaketi.

Taz: As - Sahih Minsiiratin Nabii      J.3 Uk. 173

Ndipo aliposimama Miqdad akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika wao ni Makuraishi walio na kibri, sisi tumekwisha kukuamini na kukubali na kushuhudia kwamba: Uliyoleta ni haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu, Wallahi kama utatuamrisha kuingia katika pori lenye miba Wallahi tutaingia pamoja na wewe. Wallahi hatukwambii walivyomwambia Mussa wana wa Israeli kuwa: Nenda wewe na Mola wako mkapigane, sisi tutakaa hapa. Lakini tunasema: Nenda wewe na Mola wako mkapigane sisi tutapigana pamoja naye.

Akasimama Saad akasema: "Wewe (ni zaidi ya) baba yangu na mama yangu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika sisi tulikwisha kukuamini na kukubali, na tumeshuhudia kwamba: Uliyoleta ni haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu, basi tuamrishe (tufanye) unalotaka. Wallahi kama utatuamrisha kuingia katika bahari Wallahi tutaingia pamoja na wewe, basi tupeleke kwa msaada wa Mwenyezi Mungu. Mtukufu Mtume (s.a.w.) baada ya kusikia ahadi za mabwana hawa mashujaa na waaminifu, uso wake ukakunjuka na moyo wake ukafurahi sana.

Taz: As - Sahih Minsiiratin Nabii   J.3 Uk. 174 - 175
Almizan fyitafsiri Qur-an    J.9 Uk.22 - 23