1- Yaillahi ya Majidi, Tunakupa shukurani
Msalie Muhammadi, Na watu wake nyumbani
Ndio wamejitahidi, Kwetu ikafika dini
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
2- Mrithi wa Muhammadi, Imam wetu Husseini
Kamkataa Yazidi, Kuongoza waumini
Uwanja wa Mashahidi, Akasimama Husseini
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
3- Kabila Bani Asadi, Waishi hapo jirani
Wakasogea zaidi, Kuangalia wageni
Watoto wa Muhammadi, Na masahaba sabini
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
4- Aridhi ikambidi, Kuinunua Husseini
Toka kwa Bani Asadi, Bila ya kuacha deni
Kasema Bani Asadi msiondoke kaeni
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
5- Kikundi cha Muhammadi, Ni sisi angalieni
Tunampinga Yazidi, Kuongoza waumini
Tutakufa mashahidi, Tunaomba tuzikeni
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
6- Kina mama yawabidi, Waume washaurini
Wakimhofu Yazidi, Kina mama tuzikeni
Tutasagwa sagwa hadi, Msijue huyu nani
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
7- Watoto Bani Asadi, Hamna dhambi jamani
Wakubwa wakikaidi, Watoto tufukiyeni
Twaomba mujitahidi, Mtusitiri jamani
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
8- Watu wa Bani Asadi, Ikawajaa huzuni
Watoto wa Muhammadi, Kufika machinjoni
Na vilio vikazidi kwa hutuba ya Husseini
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
9- Akina Ummar Sadi, Wakajipanga mtoni
Lengo la bin Ziyadi, Afe na kiu Husseini
Ni agizo la Yazidi, Mwana Abu Sufiyani
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
10- Abbasi kajitahidi, Visima kuchimba chini
Na ukame umezidi, Hakuna maji jamani
Ni vilio vimezidi, Kiu na njaa kambini
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
11- Husseini ikambidi anasihi wahaini
Mwamjuwa Muhammadi, Ambaye kaleta dini
Watoto wa Muhammadi, Nimebakiya Husseini
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
12- Mwamkubali Yazidi, Awatiye utumwani
Kamanda Ummar Sadi, Ni sahaba masikini
Akarusha makusudi, Mshale kwa waumini
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
13- Ajigamba na kunadi jamani shuhudiyeni
Ni mimin Ummar Sadi nashambuliya mwanzoni
Kwa bwana bin Ziyadi tukirudi mwambiyeni
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
14- Kupigana yawabidi wafuasi wa Husseini
Zuhair na Saidi wakamkinga Husseini
Walipigana Jihadi, Kuisalimisha Dini
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
15- Wote wakafa shahidi, Kumnusuru Husseini
Maiti za mashahidi, Kazikusanya Husseini
Wamekufa mashahidi,Sahaba wote jamani
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
16- Watoto wa Muhammadi, Wakaingiya vitani
Wanajeshi wa Yazidi, Wakafa wengi vitani
Watoto wa Muhammadi, Kamwe hawawezekani
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
17- Ni kiu imewazidi na njaa matumboni
Hawakujali idadi ya maaduwi jamani
Kwa uchache wanazidi maelfu thelathini
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
18- Kikundi cha Muhammadi, Wachache sana jamani
Tukizidisha idadi, Hawafiki themanini
Kwa hapa inanibidi, Nipafanye kituoni
Shahidi wa Mashahidi, Imam wetu Husseini.
Shairi na: Juma S. Magambilwa