KIFO CHA SUKAINA.


1- Kwa jina la Subuhana, shairi nawaleteya
Babu yake Sukaina, Mtume namsaliya
Amani ya Maulana, inyumbani kwa Nabiya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

2- Maelezo yenye kina, mmekwisha yasikiya

Yazidi huruma hana, mnyama alotimiya
Ikabaki Sukaina, kutwa kucha analiya

Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

3- Baada ya kupambana, dini kuipiganiya

Tumekwisha ambizana, mengi yaliyotokeya
Zainul Abidina, kitandani auguwa
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

4- Maiti zarundikana, Zainabu analiya

Pamoja na Sukaina, nguvu zimewaishiya
Lakulifanya hawana, adui kawakamiya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

5- Huyu hapa Sukaina, nikikumbuka naliya

Kama vile namuona, adui kawakamiya
Ameteseka Sukaina, na Yazidi Muawiya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

6- Tumjue Sukaina, mwana wa Hussein piya

Miaka ya Sukaina, nne haikutimiya
Akili za Sukaina, zashinda walokomaa
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

7- Kitendo cha Sukaina, nikikumbuka naliya

Wakati wa kuagana, na Hussein ameliya
Kumuona Sukaina, Farasi kamzuwiya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

8- Hussein alipoona, Farasi amgomeya

Ndipo kataka kuona, nini kinamzuwiya
Kumbe ni Kisukaina, safari chaizuwiya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

9- Vikono vya Sukaina, huwezi kutarajiya

Farasi vimembana, Farasi akatuliya
Imam alipoona, kaliya sana kaliya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

10- Kamwambiya Sukaina, huzuni unanitiya

Mimi lakufanya sina, vitani naelekeya
Binti yangu tulizana, ingawa nitauwawa
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

11- Utaliya sanasana, kwa hivi sasa tuliya

Vituko mtaviona, nakuomba vumiliya
Aduwi adabu hana, kwa watoto wa Nabiya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

12- Imam akakazana, vitani aelekeya

Njaa ya muuma sana, kiu inamsumbuwa
Imam akapambana, hadi alipouliwa
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

13- Kabaki ya Sukaina, Hemeni amebakiya

Tumboni chakula hana, kiu inamsumbua
Japo maji ayaona, adui kayazuwiya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

14- Muda si mrefu sana, Farasi akarejeya

Farasi amelowana damu mbichi nakwambiya
Ni mwanzo wa Sukaina, uyatima kuingiya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

15- Punde tu wakayaona, yale majitu mabaya

Yakitukanatukana, kambia wakaivamiya
Zainabu nguvu hana, mali zikakwapuliwa
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

16- Zainul Abidina, Kitandani auguwa

Sikiyo la Sukaina, aduwi kalipasuwa
Hereni za Sukaina, wakapata kukwapuwa
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

17- Hema wamechanachana, kwa moto wakalipuwa

Zainabu akaona, Sukaina kapoteya
Wamemtafuta sana, wapi ameelekeya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

18- Mwishowe wakamuona, maiti kakumbatiya

Kaburuzwa Sukaina, Iraki hadi Siriya
Kikundi cha waungwana, mateka chachukuliwa
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

19- Kikundi cha Sukaina, Shamu kilipoingiya

Wakadhalilishwa sana, pamoja na kuzomewa
Walikandamizwa sana, walipofika Siriya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

20- Gerezani Sukaina, taabu hakuvumiliya

Na nguvu akawa hana, akafariki duniya
Huzuni imenibana, Beti hii naishiya
Kateseka Sukaina, nikikumbuka naliya

Shairi na: Juma S. Magambilwa