HISTORIA YA EID AL - GHADIIR.

Bismmillah Rahmani Rahim

Amesema Mwenyezi Mungu (s.w.t):

"Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hukufikisha, basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu, hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafakiri."

(Qur'an: 5:67)
 
Eid Al-Ghadiir ilikuwa siku ya mwezi 18 wa Dhulhijja 10, siku ambayo Mtume (s.a.w.w) aliutangaza uongozi wa Uislam na Waislam baada ya yeye kuondoka duniani. Uislam umeifanya siku hii ni siku ya Eid kwa kuwa ndiyo siku ambayo dini ilikamilika kwa tangazo hilo.

Imam Ja'afar Swadiq (a.s) aliulizwa, je! Waislam wana Eid nyingine isiyokuwa ya mfunguo wa kwanza na mfungo wa tatu na siku ya Ijumaa? Akajibu akasema ndiyo, nayo ndiyo kubwa kuliko zote, muulizaji akasema ni ipi hiyo? Akasema ni siku Mtume (s.a.w.w) alimtangaza Imam Ali bin Abi Talib (a.s) kuwa ni khalifa na kiongozi baada yake.
Mtume (s.a.w.w) amesema: " Yoyote yule niliyekuwa mimi natawala mambo yake huyu hapa Ali ndiye atakayetawala mambo yake, ewe  Mwenyezi Mungu kuwa na atakayekuwa naye na mpige atakayempinga yeye"
Muulizaji akasema ni nini chakufanya katika siku hii? Akasema fungeni, fanyeni ibada na mtajeni sana Mtume (s.a.w.w) na watu wa nyumbani kwake.
Na Mtume (s.a.w.w) alimuamrisha Imam Ali bin Abi Talib (a.s) aifanye kuwa ni siku ya Eid.

UMUHIMU WA UONGOZI KATIKA UISLAM:-

Mwenyezi Mungu kabla hajaumba waongozwa alifikiria kuumba uongozi kwanza (Sura ya pili Aya 30) hii ni kuonyesha umuhimu wa suala la uongozi na nafasi yake katika jamii, jamii ya Kiislam duniani imepoteza muelekeo na malengo makuu ya dini yao kwa kukosa uongozi bora au hata kutokuwa nao kabisa jambo ambalo siyo sahihi na haliendi sambamba na mafundisho ya dini hi tukufu, kukosa uongozi bora ni kufeli katika kila mipango yetu ya siri na dhahiri, kukosa uongozi ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislam. Ebu tujiulize hivi kiongozi wetu wa sasa hapa duniani ni nani? Ni nani kiongozi wetu hapa chini ambaye watu wote tunamsikiliza na kumtii na kumuheshimu? Na nani kiongozi wetu anayeiona jamii inaharibika na kuipa muongozo bora wa Kiislam? Waislam kutokukubaliana na uongozi aliyoweka Mtume (s.a.w.w) enzi za uhai wake ndiko kulikosababisha Waislam tufikie hapa tulipo.
Kwa upande wa Madhihabu ya Shia Ithna Ashariyyah siku hii tumeifanya ni sikukuu kubwa kwa sababu ya kuliona suala la uongozi wa umma ni suala nyeti kabisa na lenye nafasi ya kwanza katika jamii yeyote inayotaka maendeleo, na ndiyo maana tunaikumbuka kila mwaka na tutaendelea kufanya hivyo pale Mwenyezi Mungu anapotupa nguvu na afya njema juu ya hilo, tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe afya na uwezo wa kulitangaza hilo.

HITIMISHO:-

Tukio hili lilitokea katika mwaka wa kumi wa Hijria tarehe kumi na nane mfungo wa tatu, ambapo Mtume (s.a.w.w) baada ya kumaliza Hijja yake ya mwisho wakati anarudi Madina alisimama hapo mahali panaitwa Ghadiir Khum na kutoa tangazo la uongozi wa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) baada yake.

Kwa hiyo basi tukio la Ghadiir Khum ni tukio ilililobeba ujumbe mkubwa na muhimu sana kwa umma wa Kiislam, ni tukio ambalo wanahistoria wanaona kuwa ni hitimisho la kazi ya utume, izingatiwe kwamba tukio la Ghadiir Khum ni ukweli wa Kihistoria uliothibiti ambao hautiliwi shaka ila kwa uchache wa elimu na maarifa ya dini.

YALIYO SUNNA KUFANYA SIKU HII:-
1- Kufunga
2- Kuoga
3- Ziyara ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s)
4- Kuswali rakaa mbili za Sunna
5- Kusoma dua Nudba
6- Kuwapongeza waumini kwa siku hii tukufu
7- Kusoma dua maalumu zilizoko katika kitabu cha mafaatihu Al- Jinani. Uk 423

Taz:
1-Tafsir Kabiir
2-Tafsir Naysaabur
3-Tarekh Baghdad