Katika Uislamu elimu imepewa kipaumbele sana. Aya
ya kwanza katika Qur’an imesisitiza kuhusu elimu na masomo na umuhimu wa
kalamu. Umuhimu huu ni mkubwa kiasi kwamba Uislamu unasema ni faradhi au lazima
kwa Muislamu mwanaume na mwanamke kutafuta elimu. Riwaya za Kiislamu pia
zinamuusia mwanadamu kutafuta elimu na masomo hadi kwenye maeneo ya mbali zaidi
duniani. Mbali na hayo, Uislamu unasema utafutaji elimu unapaswa kuendelea
katika kipindi chote cha maisha ya Mwanadamu. Mtume Mohammad (S.a.w.w) amesema:
“Tafuteni elimu kutoka susu hadi kaburini.” Moja ya sababu ambazo zimepelekea
Uislamu kuzingatia sana suala la elimu ni hii kuwa elimu hufungua milango ya
ujuzi na kumuwezesha mwanadamu kupata maarifa zaidi kumuhusu Mwenyezi Mungu.