KUSUJUDU JUU YA UDONGO

Bismillah Rahmanr Rahiim


Wanachuoni wa Kishia wamekubaliana juu ya kauli inayohusu ubora wa kusujudu juu ya ardhi kutokana na mapokezi wanayopokea kutoka kwa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), mapokezi hayo ni kauli ya babu yao ambaye ni Mtume wa Mwenyeezi Mungu aliposema:
                           “Bora ya Sijda ni (kusujudu) juu ya ardh”.

Na katika mapokezi mengine (amesema), “Sijida hajuzu isipokuwa juu ya ardhi au kile kilichooteshwa ardhini kisicholiwa wala kuvaliwa”. Na kwanye kitabu kiitwacho ‘Wasailus-Shia’ amesimulia kutoka kwa Muhammad bin Ali bin Hussain kwa Isnadi yake, kutoka kwa Hisham bin Al-Hakam kutoka kwa Abdillah (a.s) amesema: “Kusujudu juu ya ardhi ni bora kwani kunazidisha unyenyekevu, na unyenyekevu (ufanywe) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu”. Na ndani ya mapokezi mengine kutoka kwa Muhammad bin Al-Hassan kwa Isnad yake kutoka kwa Is’haq bin Al-Faali kuwa yeye alimuuliza Abu Abdillah (a.s) kuhusu kusujudu juu ya mkeka na jamvi lilifumwa kwa matete, akasema, “Hapana ubaya, na kusujudu juu ya ardhi kwangu mimi ni bora zaidi, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa akipenda hivyo (yaani) kuweka bapa lake la uso ardhini, basi nami nakupendelea wewe kila alichokuwa akikipenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w)” Ama wanachuoni wa KISUNNI wao hawaoni vibaya kusujudu juu ya mabusati na mazulia japokuwa ilivyo bora kwao ni kusujudu juu ya majamvi. Na kama baadhi ya riwaya ambazo amezisibitisha Bukhar na Muslim ndani ya Sahihi zao (riwaya) ambzo zinasisitiza kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa na mswala uliotengenezwa kwa makuti akisujudiajuu yake. Muslim amethibitisha ndani ya Sahihi yake katika Kitabul-Haidh kutoka kwa Yahya na Abubakr bin Abi Shaibah, kutoka kwa Abu Muawiyyah kutoka kwa Al-Aa’mash, naye kutoka kwa Thabiti bin Ubaid kutoka kwa Qasim bin Muhammad, naye kutoka kwa Aisha amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) aliniambia, nichukulie jamvi langu humo msikitini, Aisha akasema, nikamwambia mimi ninahedhi, Mtume akasema: Bila shaka hedhi yako haiku mkononi mwako”.

Taz: Haidh Ra’asa Zaujih). Sunan Abi Dawud J. 1 uk 68 (Babul-Haidh Tanawul Minal-Masjid)
Sahihi Muslim J. 1uk 168. Babu-Jawaz Ghaslil

Sasa Muslimu anasema, Al-Khumrah ni kifaa kidogo cha kusujudia kwa kiasi cha kutosha kusujudia juu yake. Na miongoni mwa mambo ambayo yanatujulisha kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa akipenda kusujudu juu ya ardhi ni mapokezi aliyothibitisha Bukhari ndani ya Sahihi yake kutoka kwa Abu-Said Al-Khudri (r.a) kwamba, “Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alikuwa akikaa itikafu katika kumi la kati ndani ya mwezi wa Ramadhani. Basi kuna mwaka Fulani alikaa itikafu mpaka ilipofika usiku wa tarehe ishirini na moja nao ni usiku ambo asubuhi yake anatoka katika itikafu yake, akasema, yeyote aliyekuwa akikaa itikafu pamoja nami, basi na akae itikafu kumi la mwisho kwa hakika usiku huu nilioteshwa kisha nikasahaulishwa na uliniona vile nikisujudu katika maji na tope, basi utafuteni katika kumi la mwisho na muutafute katika (tarehe za witri). Mvua ilinyesha usiku huo na msikiti ulikuwa wa hema babi msikiti ukavuja, na macho yangu yalimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) juu ya uso wake kuna alama ya maji na tope asubu ya tarehe ishirini na moja”

Taz: Sahihi Bukhar J. 2 uk. 256 (Babul-itikaf-Fil-A’shril-Awa’khiri).

 Pia miongoni mwa mambo yanayotujulisha ni kwamba, Masahaba walikuwa wakiboresha kusujudu juu ya ardhi, na wakifanya hivyo mbele ya Mtume (s.a.w.w) kama alivyothibitisha Imam An-Nasai ndani ya Sunan yake katika mlango wa “Tabridul-haswa Lis-Sujud Alaiha” akasema” “Ametueleza Qataybah amesema, ametusimulia Ubba’d kutoka kwa Muhammad bin Amr kutoka kwa Said bin Ali-Harith naye kutoka kwa Jabir bin Abdillah amesema: “Tulikuwa tukisali pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) sala ya adhuhuri, basi nikachukua gao la changarawe katika kiganja changu kupoza kisha huligeuzia kwenye kiganja kingine ninaposujudu huliweka gao hilo kwa ajili ya paji langu la uso”.

Taz: Sunan Al-Imam An-Nasai J. 2 uk. 204 (Babu Tabridul-Haswa Lis-Sujud A’laih).

Zaidi ya yote hayo, ni kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amesema: “Ardhi imefanywa kwa ajili yangu kuwa ni mahala pa kusujudia na tahara”.
Taz: Sahihi Bukhar J. 1 uk. 86 (Kitabu-Tayammum). Na vile vile amesema: “Ardhi yote tumefanyiwa kuwa ni mahala pa kusujudia na udongo wake ni tahara”.

Taz: Sahihi Muslim J. 2 uk. 64 (Kitabul-Masajid Wamawa-dhiu’s-Salah).

Basi ni vipi MASUNNI wanakuwa na chuki dhidi ya MASHIA kwa kuwa tu wanasujudia juu ya ardhi badala ya kusujudu kwenye mabusati. Na ni vipi mambo yanafikia kiasi cha kuwakufurisha na kuwakejeli na kuwazulia kwamba wao (Mashia) ni wanaabudu sanamu? Na vipi wanawapiga (Mashia) huko Saudi Arabia kwa kuwa tu kumepatikana Turba (Udongo) ndani ya mifuko yao au mabegi yao? Je, huu ndiyo Uislamu jamani unaotuamuru kuheshimiana sisi kwa sisi na kutokumdharau Muislamu anayempwekesha Mwenyezi Mungu, (Muislamu) ambaye anashuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, anasali, anatoa zaka na kufunga Ramadhani na kuhiji Makka. Je, inaingia akilini kwamba Mashia wanavumilia taabu hizo na kupata hasara na kuja kuhiji kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu na kuzuru kaburi la Mtume (s.a.w.w) na hali ya kuwa wanaabudu jiwe kama wanavyopenda baadhi ya watu kufikiria hivyo? Basi je, Masunni hawatosheki na kauli ya Shahidi Muhammad Baqir As-Sadr ambayo nimeinakili hihitwayo, “Thummah-Tadaytu” wakati nilipomuuliza juu ya Turbah akasema: “Sisi tunasujudu juu ya ardhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na iko tofauti baina ya kusujudu juu ya Udongo na kusujudia udongo”!! Na ikiwa Shia anachukua tahadhari ili kusujudu kwake kuwe na tahara na kunakokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu, na anafuata maamrisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na Maimamu watakatifu kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.w) na hasa katika zama zetu hizi ambazo Misikiti mingi imekuwa ikitandikwa mabusuti na sehemu zingine ikitandikwa vitu viitwavyo, “Maquette” kitu ambacho hakijulikani utengezwaji wake kwa Waislam wengi na hakitengenezwi katika nchi za Kiislam na huenda baadhi ya vitu hivyo havifai kusujudu juu yake, basi je hivi ni haki kwetu sisi kumpuuza Shia anayechunga kusihi kwa sala yake na kumtuhumu ukafiri na ushirikina kwa Shubha isiyo ya kweli.? Na Shia anayetuhumiwa kwa mambo ya dini yake na hasa hasa kwa sala yake ambayo ndiyo nguzo ya dini, utamuona (akitaka kusali) anavua mkanda wake na anavua saa yake kwa kuwa mkanda wa saa hiyo ni wa ngozi ambayo hafahamu ilikotoka. Na wakati mwingine (Shia huyu) huvua suruali yake ili aswali hali ya kuwa amevaa pajama, na yote hayo ni kwa ajili ya kuwa na tahadhari na kuonyesha umuhimu wa kisimamo chake kitukufu mbele ya Mwenyezi Mungu ili asimkabili Mola wake kwa kitu anachokichukia. Basi je, hivi mtu huyu anastahiki kejeli kutoka kwetu na kumpuuza, au anastahiki heshima na kumtukuza? Hii ni kwa kuwa yeye amevitukuza vitambulisho vya Mwenyezi Mungu. “Na yeyote mwenye kuvitukuza vitambulisho vya Mwenyezi Mungu, basi jambo hilo ni katika uchaji wa moyo”. “Enyi waja wa Mungu mcheni Mwenyezi Mungu na mseme kauli zenye msimamo”.

Na kama isingalikuwa juu yenu fadhila ya Mwenyezi Mungu na Rehma yake katika dunia na akhera, bila shaka ingalikupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyoyashughilikia. Pindi mnapotangaza kwa ndimi zenu na mnasema kwa vinywa vyenu msilolijua na mnadhani ni jambo jepesi kumbe mbele ya Mwenyezi Mungu ni jambo kubwa kabisa (Qur’an, 24:14)