KAMPENI YA "NIMR HATASAHAULIKA", YAANZA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII SAUDI ARABIA.


Wanaharakati wa Saudi Arabia wameanzisha kampeni iliyopewa jina la "Nimr Hatasahaulika" katika harakati ya kumkumbuka na kumtetea mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo Sheikh Nimr Baqir al Nimr aliyeuawa na utawala wa kifalme wa Saudia mwaka jana wa 2016. Wanaharakati hao pia wamewataka wanaharakati wenzao kuunga mkono kampeni hiyo.
Sheikh Baqir Nimr alitiwa nguvuni mwezi Julai mwaka 2012 kufuatia maandamano na malalamiko makubwa ya kudai haki na uadilifu ya watu wa eneo la Qatif mashariki mwa Saudi Arabia lenye Waislamu wengi wa madhehebu ya Shia. Tarehe 15 Oktoba mwaka 2015 Sheikh Nimr alihukumiwa kifo kwa kukatwa kichwa kwa panga na kusulubiwa kadamnasi kwa tuhuma ambazo hazikuwa na msingi eti za kuhujumu usalama wa taifa na kupiga vita utawala wa nchi hiyo. Hukumu ya kifo dhidi ya msomi huyo wa Kiislamu na wenzake 46 waliotambulishwa kuwa ni magaidi, ilitekelezwa tarehe 2 Januari 2016 na kulaaniwa na mataifa ya Kiislamu, nchi na jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu.
Mtaalamu wa masuala ya haki za binadamu wa Bahrain, Baqir Darwish anasema: "Kadhia ya kuuliwa shahidi Sheikh Nimr Baqir al Nimr ilikuwa mtihani mkubwa kwa jamii ya kimataifa. Inasikitisha kwamba, jamii ya kimataifa ilifeli katika mtihani huo kwa kushindwa kuzuia mauaji ya msomi huyo wa Saudia na iliupatia zawadi utawala wa Aal Saud kwa kutenda jinai hiyo", mwisho wa kunukuu.
Utawala wa kifalme wa Saudia umezidisha mashinikizo na ukandamiza dhidi ya raia wa nchi hiyo hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia, na jeshi la nchi hiyo kwa sasa linafanya mashambulizi makali zaidi kuwahi kushuhudiwa dhidi ya Mashia wa mashariki mwa nchi hiyo. Pamoja na hayo malalamiko yanayoendelea kufanywa na Wasaudia dhidi ya jinai ya kumuua shahidi Sheikh Baqir Nimr ni kielelezo kwamba, ukandamiza huo si tu kwamba umezima na kupunguza malalamiko na upinzani wa wananchi, bali pia umeyapanua zaidi hadi kwenye mitandao ya kijamii.
Licha ya mbinyo na ukandamizaji huo dhidi ya wapinzani nchini Saudia, harakati za kudai uadilifu zinazidi kuongezeka kila siku, suala linaloonesha kwamba, vitisho, mauaji na kufungwa jela havijafanikiwa kuzima sauti na harakati za kupigania haki, uhuru wa kuabudu na demokrasia. Itakumbukwa kuwa, Sheikh Baqir al Nimr pia alisimama kidete hata alipokuwa katika jela za utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na hakusalimu amri hadi alipouliwa. Kuendelea kwa upinzani na malalamiko hayo ya wananchi licha ya ukatili na mauaji hayo kuna maana kwamba, watu wa Hijaz wameazimia ipasavyo kwa ajili ya kutimiza malengo yao na kuuondoa utawala wa kidikteta na kidhalimu unaotawala nchi hiyo.
Ali Raslani ambaye ni mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu wa Lebanon anasema: "Licha ya kupita karibu mwaka mmoja na nusu tangu kuuawa shahidi Sheikh Nimr Baqir al Nimr tunaona kuwa, msomi huyo anakumbukwa mahala pote, na roho yake ya kupambana na sera za kuwatenganisha Waislamu na kukabiliana na dhulma zinazitia hofu tawala za watenda jinai".