MLIPUKO UMETOKEA MSIKITI WA KISHIA KATIKA MJI WA QATIF.


Watu wasio pungua 22 wamefariki dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko mkubwa katika msikiti wa Kishia mjini Qatif, mashariki mwa Saudi Arabia. Mlipuko huo ambao ni shambulio la kujitolea muhanga umetokea katika Msikiti wa Imam Ali AS katika kijiji cha al-Qadeeh mjini Qatif. Taarifa ya vyombo vya usalama imesema kuwa, mtu aliyekuwa amejifunga mabomu alijilipua msikitini hapo huku waumini wapatao 150 wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Sala ya Ijumaa. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia ameziambia duru za habari kwamba, magaidi wawili walishiriki katika operesheni hiyo ya kujitolea muhanga katika Msikiti wa Imam Ali AS.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, majeruhi ambao baadhi yao walikuwa na hali mbaya wamepelekwa hospitali ya Mudhar na hospitalii kuu ya Qatif. Eneo la al-Qadeeh ambalo liko kaskazini magharibi mwa mkoa wa Mashariki wa Qatif wakazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.