KIONGOZI MUADHAMU AONANA NA RAIS WA IRAQ.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo ameonana na Rais wa Iraq na kusisitiza kuwa, nchi hiyo ni yenye taathira katika masuala ya eneo la Mashariki ya Kati kutokana na umuhimu na nafasi yake ya kipekee.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei aidha amesema katika mazungumzo yake hayo na Rais Fuad Ma'asum wa Iraq pamoja na ujumbe alioandamana nao, kuwa, kutokana na nafasi yake ya kipekee, Iraq inaweza kuwa na taathira kubwa katika nchi za Kiarabu na za Kiislamu na inabidi uwezo na nafasi hiyo itumiwe vizuri kadiri inavyowezekana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq ni mkubwa na ni wa kina na amekaribisha juhudi za kupanua uhusiano wa nchi hizo mbili kadiri inavyowezekana. Aidha amesema, uhusiano wa hivi sasa wa Iran na Iraq ni wa kipekee kabisa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja njama za maadui wa Uislamu dhidi ya Syria kuwa ni hatari kubwa sana na kusisitiza kwamba, maadui wana nia ya kueneza vurugu na kuhakikisha kuwa ukosefu wa amani unadumu nchini Syria ili kulifanya eneo hili zima lisiwe na utulivu.
Ayatullahil Udhma Khamenei amegusia pia hali ya kusikitisha ya nchini Yemen na kusisitiza kuwa, Wasaudia wamefanya kosa kubwa la kuivamia na kuishambulia kinyama Yemen na bila ya shaka yoyote madhara ya jinai wanazofanya huko Yemen yatawarejea wenyewe.
Ametaka mashambulio na mauaji dhidi ya wananchi wa Yemen yakomeshwe mara moja na kuongeza kwamba, fikra isiyo ya busara na ya kijahili ndani ya serikali ya Saudia ndiyo inayochukua maamuzi kuhusiana na Yemen.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Fuad Ma'asum wa Iraq kwa mara nyingine tena ameishukuru Iran kwa kuwasaidia wananchi na serikali ya nchi yake katika wakati mgumu kabisa wa uvamizi wa kundi la kigaidi la Daesh na kuongeza kuwa, Daesh ya Iraq na Daesh ya Syria hazina tofauti yoyote kwani kundi hilo la kigaidi ni hatari kwa watu wote.

IRAN: HATURUHUSU KUPEKULIWA MELI YETU IENDAYO YEMEN.

Iran imesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haitoiruhusu nchi yoyote ile inayoshiriki katika mashambulizi dhidi ya wananchi wa Yemen iipekuwe meli yake ya mizigo inayowapelekea misaada ya kibinadamu wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.
"Hatutoziruhusu kamwe nchi zinazohusika na vita vya Yemen kuipekuwa meli iliyo na misaada ya kibinadamu ya Jamhuri ya Kiislamu," amesema Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bi Marzie Afkham, leo Jumatano.
Ameongeza kuwa, "mzingiro wa kiadui" uliowekwa dhidi ya Yemen na nchi zilizoivamia nchi hiyo kwa siku 50 sasa umeharibu kabisa maisha ya watu wa nchi hiyo na kuonya kuhusu maafa ya kibinadamu ya taifa hilo maskini.

Bi Afkham ameongeza kuwa, katika siku za hivi karibuni Iran imefanya mazungumzo na taasisi za kimataifa zikiwemo zenye mfungamano na Umoja wa Mataifa kuhusiana na njia za kupeleka misaada ya haraka huko Yemen kama vile chakula na madawa na imeanza kupeleka misaada kwa nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita baada ya kufanya mazungumzo na taasisi hizo. chanzo cha habari: kiswahili.irib